Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Kujibadili Rangi wa Ngisi Anayeitwa Cuttlefish

Uwezo wa Kujibadili Rangi wa Ngisi Anayeitwa Cuttlefish

NGISI anayeitwa cuttlefish ana uwezo wa kujibadili rangi na kujificha hivi kwamba asiweze kuonwa na mwanadamu. Kulingana na ripoti moja, ngisi hao “wanafahamika kuwa na rangi mbalimbali na wanaweza kubadili rangi hizo kwa njia ya kustaajabisha.” Wanafanyaje hivyo?

Fikiria hili: Ngisi huyo hujibadili rangi kwa kutumia chembe fulani ndogo za pekee zilizo chini ya ngozi yake. Chembe hizo huwa na vifuko vilivyojaa rangi mbalimbali vilivyozungukwa na misuli midogo sana. Ngisi huyo anapotaka kujibadili rangi ili ajifiche, ubongo wake hutuma taarifa ya kukaza misuli inayozunguka vifuko hivyo. Kisha vifuko hivyo na rangi zilizo ndani yake hutanuka na rangi ya ngisi huyo hubadilika mara moja. Mbali na kuutumia uwezo huo ili kujificha ngisi huyo huutumia kuwavutia ngisi wengine na labda hata kuwasiliana nao.

Wataalamu katika Chuo Kikuu cha Bristol, Uingereza, walitengeneza ngozi kama ya ngisi huyo. Waliweka visahani vya mpira mweusi katikati ya vitu vidogo vinavyotenda kama misuli ya ngisi huyo. Watafiti hao walipounganisha umeme kwenye ngozi hiyo, misuli hiyo ilitanua visahani hivyo vyeusi na kubadili rangi ya ngozi hiyo.

Utafiti uliofanywa kuhusu misuli ya ngisi huyo unaweza kutumiwa kutokeza nguo ambazo hubadilika rangi upesi sana. Jonathan Rossiter alifafanua misuli hiyo kuwa “laini na imebuniwa kwa ustadi wa hali ya juu,” na akasema kwamba huenda siku moja watu watavaa nguo zilizobuniwa kwa kutegemea muundo wa ngozi ya cuttlefish zinazoweza kubadilika rangi—iwe ni kwa ajili ya kujificha au kama mtindo wa mavazi.

Una maoni gani? Je, uwezo wa ngisi anayeitwa cuttlefish wa kujibadili rangi ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?