Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Nyuzinyuzi za Kome wa Baharini

Nyuzinyuzi za Kome wa Baharini

KOME wa baharini hujishikiza kwenye miamba, vipande vya mbao, na meli kama chaza wanavyofanya. Hata hivyo, tofauti na chaza ambao hujishikiza kwa nguvu, kome huning’inia kwa kutumia nyuzinyuzi nyembamba zilizo kwenye mwili wao. Ingawa nyuzinyuzi hizo humsaidia kula na kuhama kwa urahisi, huenda zikaonekana kuwa dhaifu sana kumlinda asisombwe na mawimbi makubwa ya baharini. Nyuzinyuzi hizo zinawasaidiaje kome kuning’inia bila kupelekwa na mawimbi?

Fikiria hili: Sehemu moja ya nyuzinyuzi hizo ni ngumu, na nyingine ni laini. Watafiti wamegundua kwamba uwiano sahihi kati ya sehemu ngumu na laini ya nyuzinyuzi za kome, yaani, asilimia 80 ya sehemu ngumu na 20 ya sehemu laini, ndio huwasaidia kujishikiza bila kupelekwa na maji. Hivyo, nyuzinyuzi hizo humwezesha kustahimili mawimbi yanapomsukuma huku na huku.

Profesa Guy Genin anasema kwamba matokeo ya utafiti huo ni yenye “kustaajabisha.” Anaongeza hivi: “Uwezo wa ajabu wa viumbe hawa unategemea jinsi ambavyo sehemu laini imeunganishwa kwa makini sana na ile sehemu ngumu.” Wanasayansi wanaamini kwamba kuiga jinsi nyuzinyuzi za kome zinavyofanya kazi kunaweza kutumiwa kushikisha vifaa kwenye majengo na kwenye vyombo vya majini, kuunganisha kano kwenye mifupa, na kuunganisha sehemu ya mwili iliyofanyiwa upasuaji. Profesa J.  Herbert Waite, wa Chuo Kikuu cha California jijini Santa Barbara, Marekani, anasema hivi: “Kuna hazina nyingi sana katika uumbaji zinazoweza kutusaidia kujifunza mambo mengi kuhusu mbinu za kushikisha vitu.”

Una maoni gani? Je, nyuzinyuzi za kome wa baharini zilijitokeza zenyewe? Au zilibuniwa?