Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hariri—Nyuzi Bora Zaidi

Hariri—Nyuzi Bora Zaidi

Hariri—Nyuzi Bora Zaidi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI

BAADHI ya nguo maridadi zaidi ulimwenguni kutia ndani kimono ya Japani, sari ya India, na hanbok ya Korea, zinafanana katika njia fulani. Mara nyingi, nguo hizo hutengenezwa kwa hariri, kitambaa kinachong’aa ambacho imesemekana kwamba ndicho chenye nyuzi bora zaidi. Kuanzia wafalme walioishi zamani hadi watu wa kawaida wanaoishi leo, watu ulimwenguni wamevutiwa na uzuri wa hariri. Lakini hariri haijawa ikipatikana kwa urahisi sikuzote.

Zamani za kale China peke yake ndiyo nchi iliyotokeza hariri. Watu wengine hawakujua siri ya kutokeza hariri na mtu yeyote nchini China aliyetoboa siri hiyo angeweza kuuawa kwa kuwa msaliti. Kwa hiyo, haishangazi kwamba hariri ilikuwa ghali sana. Kwa mfano, katika Milki yote ya Roma hariri ilikuwa na thamani sana kama dhahabu.

Hatimaye, Uajemi ilisimamia hariri yote iliyotoka China. Lakini bado bei ya hariri ilikuwa juu na jitihada za kuwaepuka wafanyabiashara wa Uajemi hazikufua dafu. Kisha, Maliki Justinian wa Byzantium akatunga hila. Yapata mwaka wa 550 W.K., aliwapa watawa wawili wa kiume utume wa siri kwenda China. Walirudi baada ya miaka miwili. Ndani ya mikongojo yao ya mianzi walikuwa wameficha hazina iliyokuwa ikingojewa kwa hamu, yaani, mayai ya nondo wa hariri. Siri ilikuwa imefichuka. Sasa China haikuwa tena nchi pekee iliyotengeneza hariri.

Jinsi Ambavyo Hariri Hutokezwa

Hariri hutokezwa na nondo wa hariri. Kuna aina nyingi za nondo hao, lakini jina la kisayansi la nondo anayetokeza hariri bora zaidi ni Bombyx mori. Nondo kadhaa huhitajiwa ili kutengeneza vitambaa vya hariri, na hilo limetokeza ufugaji wa nondo wa hariri. Familia ya Shoichi Kawaharada, inayoishi katika Wilaya ya Gunma, Japani, ni mojawapo ya familia 2,000 hivi nchini humo ambazo bado hufanya kazi hiyo ngumu. Nyumba yao yenye orofa mbili ambayo imejengwa hasa kwa kusudi la ufugaji wa nondo wa hariri, iko juu ya mlima kwenye upande ulio na msitu wa miforosadi (1).

Nondo wa hariri wa kike hutaga mayai 500 hivi, na kila yai lina ukubwa wa kichwa cha pini (2). Baada ya siku 20 hivi, mayai hayo huangua. Nondo hao wadogo hula sana. Wao hula majani ya miforosadi usiku na mchana. Hawali majani mengine yoyote ila tu yale ya mforosadi. (3, 4). Baada ya siku 18 tu, nondo wa hariri huwa na ukubwa mara 70 zaidi ya ule wa awali, nao watakuwa wameambua ngozi yao mara nne.

Bwana Kawaharada hufuga nondo wa hariri 120,000 hivi kwenye shamba lake. Wanapokula, wao hutokeza sauti kama ya mvua kubwa inapoanguka juu ya majani. Kufikia wakati nondo wa hariri anapokomaa, anakuwa na uzito mara 10,000 ya ule wa awali! Sasa yuko tayari kusokota kifuko.

Hutokeza Hariri Kimya-Kimya

Nondo anapokomaa kabisa, ngozi ya mwili wake hubadilika na kuwa nyangavu. Hilo huonyesha kwamba yuko tayari kuanza kusokota kifuko. Nondo wanapoanza kukosa utulivu na kuanza kutafuta mahali pa kusokota vifuko vyao, wako tayari kuingizwa kwenye sanduku lililo na visehemu vingi. Wakiwa humo wao hutoa nyuzi zao nyeupe zilizo bora (5) na kujifunika kwa hariri.

Wakati huo Bw. Kawaharada huwa na kazi nyingi sana kwa kuwa nondo wa hariri wote hao 120,000 huanza kusokota vifuko vyao karibu wakati uleule. Masanduku yamening’inizwa katika safu nyingi kwenye mianya ya orofa ya pili ya nyumba yake (6).

Wakati huohuo, badiliko lenye kushangaza huwa linatukia ndani ya mwili wa nondo wa hariri. Majani ya miforosadi iliyomeng’enywa hugeuzwa kuwa aina fulani ya protini ambayo huhifadhiwa kwenye tezi mbili zenye urefu wa nondo. Protini hiyo inaposukumwa ndani ya tezi hizo, hiyo hufunikwa kwa kitu fulani kilicho kama gundi. Kabla ya kutoka mdomoni mwa nondo, nyuzi mbili za protini hiyo huunganishwa pamoja kwa gundi hiyo. Umajimaji huo unapopigwa na upepo huwa mgumu na kufanyiza uzi mmoja mwembamba.

Nondo wa hariri anapoanza kutokeza hariri huwezi kumzuia. Nondo wa hariri husokota uzi wenye urefu wa sentimeta 30 hadi 40 kwa dakika moja huku akizungusha kichwa chake wakati huo wote. Makala moja inakadiria kwamba kufikia wakati atakapokuwa amemaliza kusokota kifuko chake, atakuwa amezungusha kichwa chake mara 150,000 hivi. Baada ya kusokota uzi kwa siku mbili mchana na usiku, nondo wa hariri atakuwa ametokeza uzi wenye urefu wa meta 1,500 hivi. Urefu huo unazidi kimo cha jengo refu sana kwa mara nne hivi!

Katika juma moja tu, Bw. Kawaharada atakuwa amepata vifuko 120,000, ambavyo hatimaye vitasafirishwa hadi kiwandani. Vifuko 9,000 hivi vinahitajiwa ili kushona kimono kimoja na vifuko 140 hivi ili kushona tai, na zaidi ya vifuko 100 ili kushona skafu.

Jinsi Ambavyo Kitambaa cha Hariri Hutengenezwa

Mbinu ya kutoa hariri kwenye kifuko kwa kuizungusha kwenye kigurudumu ilianzaje? Kuna hekaya na ngano nyingi sana kuhusu jambo hilo. Moja inasema kwamba kifuko kutoka kwenye mforosadi kilianguka ndani ya kikombe cha chai cha Maliki wa kike wa China aliyeitwa Hsi Ling-Shi. Alipojaribu kukitoa, aliona kwamba kilijikunjua na kuwa nyuzinyuzi laini za hariri. Mbinu ya kutoa hariri kutoka kwenye kifuko kwa kuizungusha kwenye kigurudumu ilianzia hapo. Leo kazi hiyo hufanywa kwa mashini.

Ili vifuko vya nondo wa hariri viweze kuuzwa, lazima mabuu yaliyo ndani yauawe kabla hayajaangua. Joto hutumiwa ili kufanya hilo. Vifuko vilivyoharibika huondolewa na vile vinavyobaki huwa tayari kutolewa nyuzi. Kwanza, vifuko huwekwa ndani ya maji moto au mvuke ili kulegeza gundi inayoshikilia nyuzi. Kisha, mwanzo wa nyuzi hizo hukamatwa kwa brashi zinazozunguka (7). Ikitegemea unene unaotakiwa, nyuzinyuzi kutoka kwenye vifuko viwili au zaidi zinaweza kuunganishwa na kutokeza uzi mmoja. Uzi huo hukaushwa unapozungushwa kwenye kigurudumu. Hariri iliyotokezwa huzungushwa tena kwenye gurudumu kubwa zaidi ili kufanyiza fundo la uzi wenye urefu na unene unaohitajiwa (8, 9).

Labda umewahi kugusa kitambaa cha hariri kilichokuwa chororo na laini sana hivi kwamba ulitaka kugusa mashavu yako nacho. Ni nini hufanya kiwe chororo hivyo? Sababu moja ni kwamba gundi ambayo hufunika protini huondolewa. Hariri ambayo haijaondolewa gundi huwa ngumu na si rahisi kuitia rangi. Kitambaa cha shifoni si chororo kabisa kwa kuwa hakijaondolewa gundi yote.

Jambo lingine linalofanya kitambaa cha hariri kuwa chororo ni mara ambazo nyuzi zinazungushwa kwenye kigurudumu. Kitambaa cha Wajapani kinachoitwa habutai, ni laini na chororo. Nyuzi zake hazijazungushwa mara nyingi. Hicho huwa tofauti na kitambaa cheusi chenye mikunjo kinachoitwa crepe ambacho hutengenezwa kwa nyuzi zilizozungushwa sana.

Hatua nyingine muhimu ni kutia rangi. Ni rahisi kutia hariri rangi. Muundo wa protini ya hariri hufanya iwe rahisi rangi kupenya ndani kabisa na hivyo kufanya rangi ikolee kabisa. Isitoshe, tofauti na nyuzi zinazotengenezwa viwandani, hariri ina atomu chanya na hasi, hivyo inaweza kushika rangi yoyote vizuri. Hariri inaweza kutiwa rangi kabla au baada ya kufumwa kwenye kitanda cha kufuma (10). Kimono zinazojulikana sana za yuzen zinapotiwa rangi, picha maridadi huchorwa na kutiwa rangi kwa mkono baada ya hariri kufumwa.

Ingawa leo hariri nyingi hutokezwa katika nchi kama vile China na India, wabuni wa mitindo wa Ufaransa na Italia ndio wanaoongoza katika mitindo mbalimbali ya hariri. Bila shaka, leo nyuzi za rayoni na nailoni hutumiwa kutengeneza nguo nyingi za bei ya chini. Hata hivyo, bado hariri haina kifani. “Hata ingawa leo kuna maendeleo ya kisayansi, hariri haiwezi kutengenezwa viwandani,” anasema msimamizi wa Jumba la Makumbusho la Hariri huko Yokohama, Japani. “Tunajua kila kitu kuhusu hariri, kuanzia mpangilio wake wa molekyuli hadi muundo wake. Lakini hatuwezi kuitengeneza viwandani. Hilo ndilo mimi huita fumbo la hariri.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

JINSI Hariri ILIVYO

Ngumu: Hariri ina nguvu kama nyuzi kubwa za chuma.

Hung’aa: Hariri hung’aa kama lulu. Mng’ao huo hutokezwa na protini yake yenye tabaka mbalimbali na umbo la mche, ambalo hugawa nuru.

Haikwaruzi ngozi: Asidi amino zinazofanyiza hariri hazikwaruzi ngozi. Inasemekana kwamba hariri humlinda mtu dhidi ya magonjwa mbalimbali ya ngozi. Vipodozi fulani hutengenezwa kutokana na ungaunga wa hariri.

Hufyonza unyevu: Asidi amino na matundu madogo yaliyo katika kitambaa cha hariri hufyonza na kutoa kiasi kikubwa cha unyevu na hivyo kumfanya mtu astarehe wakati wa joto.

Haiteketei kwa urahisi: Hariri haiteketei kwa urahisi na haitoi gesi zenye sumu inapoteketea.

Hulinda ngozi: Hariri hufyonza miale ya urujuanimno na hivyo kuilinda ngozi.

Si rahisi kutokeza umeme-tuli: Kwa kuwa hariri ina atomu chanya na hasi na hufyonza unyevu, si rahisi itokeze umeme-tuli kama vitambaa vingine.

JINSI YA KUTUNZA Hariri

Kufua: Inafaa zaidi kupeleka nguo za hariri kwa dobi. Ukiamua kujifulia, tumia sabuni isiyo na kemikali kali na maji yenye joto la kadiri (karibu nyuzi 30 Selsiasi). Fua kwa wororo, usisugue wala kukamua. Usizikaushe kwa mashini, zianike.

Kupiga pasi: Unapopiga pasi nguo za hariri weka kitambaa juu yake. Piga pasi ukiielekeza kwenye nyuzi zake. Pasi iwe na joto la nyuzi 130 Selsiasi hivi. Ikiwa utatumia mvuke, tumia kiasi kidogo sana.

Kuondoa madoa: Nguo inapopata doa, weka upande wa juu ukiangalia chini juu ya kitambaa kikavu. Pigapiga kwa kitambaa chenye maji, lakini usisugue. Kisha peleka nguo kwa dobi.

Jinsi ya Kuiweka: Epuka mahali penye unyevu, penye nondo, na mwangaza. Ining’inize juu ya waya yenye sponji, au ikiwezekana iweke mahali ambapo haitakunjamana.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Vifuko vya hariri

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Photos 7-9: Matsuida Machi, Annaka City, Gunma Prefecture, Japan; 10 and close-up pattern: Kiryu City, Gunma Prefecture, Japan