Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kweli Huu ni Mti?

Je, Kweli Huu ni Mti?

Je, Kweli Huu ni Mti?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

HUENDA mibuyu minene inayokua katika maeneo kame ya Australia ikaonekana kuwa isiyo ya kawaida na hata isiyopendeza. Kwa kuwa wakati wa ukame miti hiyo humwaga matawi, mibuyu iliyokomaa haifanani kama miti badala yake inafanana na viumbe wa ajabu walioinua mikono juu. Hekaya moja ya Wenyeji wa Asili wa Australia husema kwamba mti huo ulilaaniwa na kusimamishwa chini juu!

Kwa kawaida miti hiyo inapokuwa midogo inakuwa myembamba na inavutia. Lakini kadiri inavyozeeka, mashina yake hunenepa, huchakaa, na kupata makovu. Mibuyu “huonekana kama inaugua ugonjwa fulani,” akaandika mvumbuzi George Grey mnamo 1837. Kwa nini mibuyu inatofautiana sana na miti mingine, na kwa nini inathaminiwa na kupendwa na watu wa vijijini, kutia ndani Wenyeji wa Asili wa Australia?

Jina Lililofupishwa

Mibuyu hukua kiasili barani Afrika, nchini Madagaska, na kaskazini-magharibi mwa Australia. Katika nchi nyingi, jina la mti huo, yaani, baobab, ni ndefu, lakini kwa muda mrefu Waaustralia wamefupisha jina hilo kuwa boab. Wacheshi fulani Waaustralia husema kwamba watu wanaoishi msituni walipenda sana kufupisha majina kwa sababu hawakutaka kufungua vinywa vyao kwa muda mrefu ili nzi waliokuwepo kwa wingi wasiingie. Hivyo, walifupisha jina baobab kuwa boab, na jina hilo fupi likadumu katika lugha ya wenyeji.

Mibuyu inaitwa pia miti ya panya waliokufa. Kwa nini inapewa jina mbovu hivyo? Kutoka mbali, maganda ya mbegu zake yanayoning’inia yanaonekana kama panya waliokufa waliofungiliwa juu kwa mikia yao. Pia, maua yanapokwaruzwa au kuharibiwa, yanachacha upesi, na kuwa na harufu kama ya nyama inayooza. Maua yake mazuri ni makubwa, meupe, na huwa na harufu nzuri.

Inastahimili Hali Mbaya

Mibuyu inasitawi katika maeneo ya mbali ya Kimberley, katika jimbo la Australia Magharibi na katika jimbo jirani la Nchi ya Kaskazini. Majimbo hayo huwa na majira mafupi ya mvua nyingi na majira ya ukame.

Uwezo wa mibuyu wa kuchipuka upya unajulikana sana. Mibuyu mingi inaishi kwa karne nyingi. “Hata sehemu yake ya ndani ikiteketezwa au ganda lake likiondolewa kimzunguko, mti huo hupona, na baada ya kujirekebisha, huendelea kukua,” anasema mtaalamu wa mimea D. A. Hearne. * Anaongeza hivi: “Uwezo wa kustahimili wa mti huo ni mkubwa sana hivi kwamba usipoharibiwa kabisa, utaendelea kukua kama kawaida.” Ukiwa umeazimia kuokoka, mbuyu fulani uliowekwa ndani ya sanduku la mbao ukingoja kusafirishwa ng’ambo ulipenyeza mizizi yake kupitia mianya ya sanduku hilo hadi kwenye udongo!

Mibuyu ambayo hukua kwenye vijito vilivyokauka, mabonde yenye miamba, au nchi tambarare zenye mchanga, huwa mirefu kuliko miti mingine. Mibuyu fulani katika Uwanda wa Kimberley hufikia kimo cha mita 25 au zaidi na upana karibu kama huo.

Mibuyu huwa minene kwa sababu ya kuwa na maji mengi. Kama sifongo, mbao za mbuyu ni laini, zenye nyuzi, na zinaweza kuhifadhi maji mengi sana. Baada ya kufyonza maji ya mvua, shina la mbuyu hufura sana. Msimu wa kiangazi unapoendelea, mti huo hurudia ukubwa wake pole kwa pole.

Wakati wa miezi ya baridi kali, miti fulani huokoka kwa kumwaga majani yake. Mibuyu hufanya hivyo wakati wa majira marefu ya kiangazi. Majira hayo yanapokaribia kwisha, maua huanza kuchanua na majani huota. Kwa kuwa mti huo unapoanza kuchanua watu hutambua kwamba majira ya mvua yamekaribia, nyakati nyingine wenyeji huita mti huo mmea wa kalenda.

Maua huchanua usiku tu, yanakaa kwa saa chache tu, na kuanza kunyauka baada ya jua kuchomoza. Maganda ya maua hukua na kutokeza kokwa kubwa, au vibuyu, ambavyo huanguka ardhini, hupasuka, na mbegu zake hutawanyika.

Mti wa Uzima

Kwa muda mrefu sana Wenyeji wa Kimberley wametegemea mbegu, majani, utomvu, na mizizi ya mibuyu kwa ajili ya chakula. Kabla ya kukauka, mbegu zake hufunikwa na utomvu mwororo, mweupe ambao ni mtamu. Wakati wa ukame, Wenyeji wa Asili wa Australia walitafuna mizizi na mbao zake zenye nyuzi, na kupata maji. Wakati wa majira ya mvua nyingi, nyakati nyingine wenyeji walipata maji katika mashimo yaliyo ndani ya miti hiyo na katika matawi.

Mnamo 1856, kikundi cha wavumbuzi cha Augustus Gregory waliotembelea Uwanda wa Kimberley waliposhikwa na ugonjwa wa kiseyeye, walichemsha sehemu ya ndani ya mabuyu ili kufanyiza “jemu tamu.” Kwa kuwa utomvu huo una vitamini C nyingi uliwafanya wanaume hao wapone.

Miti Inayofunua Matukio Yaliyopita

Zamani, Wenyeji wa Asili wa Australia na pia watu kutoka Ulaya waliandika ujumbe kwenye mibuyu. Mnamo 1820, chombo cha majini kilichoitwa Mermaid kilitia nanga katika pwani ya Kimberley ili kifanyiwe marekebisho. Akitii agizo la wasimamizi wa jeshi la majini lililotaka waache uthibitisho usioweza kupingwa kwamba walitia nanga katika eneo hilo, Kapteni Phillip Parker King alichonga maneno “HMC Mermaid 1820” kwenye shina la mbuyu mkubwa.

Wakati huo, mbuyu huo ambao ulikuja kuitwa Mti wa Mermaid, ulikuwa na upana wa mita 8.8. Leo, upana wake unazidi kidogo mita 12.2. Ijapokuwa leo maneno hayo hayaonekani waziwazi, bado yanawakumbusha watu kuhusu wavumbuzi hao wa mapema. Jumbe zilizochongwa kwenye mibuyu fulani mizee zinaonekana hata leo, nazo zimeonekana na watalii kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu.

Walowezi kutoka Ulaya walipofika katika Uwanda wa Kimberley, mibuyu mikubwa ilitumiwa kama ishara za barabarani, mahali pa kufanyia mikutano, na vituo vya kupiga hema katika nchi ngeni. Wafugaji waliosafiri waliruhusu ng’ombe wao wapumzike chini ya mibuyu iliyokuwa imeandikwa majina kupendeza kama vile Oriental Hotel, Club Hotel, au Royal Hotel.

Mwaka wa 1886, Wenyeji wa Asili wa Australia wenye uhasama walipoiba mashua ya mlowezi Mjerumani August Lucanus, kikundi chake kilipaswa kutembea kilomita 100 hadi mjini Wyndham. Njia ambayo wangepitia ilikuwa na mito na vijito vilivyojaa mamba. Baadaye, Lucanus aliandika kwamba kutokana na kitabu cha kumbukumbu cha mvumbuzi mmoja wa mapema, yeye na kikundi chake walijua “mahali alipokuwa amefukia zana fulani za seremala karibu na Pitt Springs chini ya mbuyu mkubwa, na kuchonga herufi za kwanza za jina lake kwenye mti huo.” Kwa kushangaza, wanaume hao waliupata mti huo na zana hizo. Kisha “wakakata na kuuangusha mbuyu mkubwa mzuri,” na kwa siku tano wakajenga mtumbwi. Ulielea vizuri, na wote wakafika salama nyumbani.

Miwili kati ya mibuyu inayojulikana sana ni ile inayoitwa Miti ya Gereza la Derby na Wyndham, majina ambayo yametokana na miji iliyo karibu. Kulingana na hekaya maarufu, miti hiyo mikubwa iliyo na mashimo, kila moja likiwa kubwa vya kutosha kuwakinga wanaume kadhaa, ilitumika kama jela katika karne ya 19. Hata hivyo, wanahistoria fulani wa kisasa wanatilia shaka madai hayo. Vyovyote vile, miti hiyo inavutia sana na inapendeza watalii.

Sanaa ya Mbuyu

Wakati fulani watu walichonga picha na jumbe kwenye mashina ya mibuyu. Hata hivyo leo, wasanii wa Australia vijijini, hawachongi miti yenyewe bali wanachonga kokwa za mbuyu zenye umbo la yai, na ambazo zinaweza kuwa na urefu wa sentimita 25 hivi na mzingo wa sentimita 15.

Baada ya kuchagua kokwa zuri mtini, msanii, akitumia kisu cha mfukoni, huchonga maumbo yenye sehemu nyingi kwenye kokwa hilo la kahawia. Michongo mingi ni ya wanyama wa eneo hilo, mandhari za uwindaji za wenyeji, na nyuso na maumbo ya wanadamu. Mara nyingi watu wanaokusanya vitu hukusanya michongo hiyo. Wanunuzi wengine wanatia ndani watalii na wenye maduka ya rejareja katika eneo hilo.

Ni kweli kwamba, huenda mbuyu si mti mkubwa au mrefu zaidi duniani. Hata hivyo, kwa sababu zake za pekee, mti huo unaohimili hali ngumu na usioweza kuharibiwa kwa urahisi ni wenye manufaa sana huko Australia vijijini, unamletea Muumba sifa, na huenda unaonyesha kwamba yeye ni mcheshi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Kuondoa ganda kimzunguko humaanisha kuondoa ganda kuzunguka shina la mti. Hilo huzuia utomvu usisambazwe na hivyo miti mingi hufa.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Maua huchanua usiku na kunyauka baada ya saa chache tu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kokwa la mbuyu lililo na mchongo wa mjusi