Hamia kwenye habari

Jengo linaloitwa Palace of Justice ambapo Mahakama Kuu ya Italia huendesha shughuli zake jijini Rome

FEBRUARI 9, 2021
ITALIA

Mahakama Kuu ya Italia Yawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Katika Kesi Inayohusu Matibabu

Mahakama Kuu ya Italia Yawaunga Mkono Mashahidi wa Yehova Katika Kesi Inayohusu Matibabu

Mahakama Kuu ya Italia ilitoa uamuzi uliomuunga mkono Shahidi wa Yehova kuhusu haki yake ya kufanya maamuzi yanayohusu matibabu. Desemba 23, 2020, Mahakama Kuu ilikubali kwamba wagonjwa wote wana haki ya kujiamulia matibabu watakayopata, kutia ndani haki ya kujichagulia matibabu yasiyopingana na dhamiri yao ya kidini.

Kesi hiyo ilihusu jambo lenye kusikitisha lililotokea katika mwaka wa 2005, wakati ambapo madaktari walikiuka haki za dada yetu mmoja. Kabla ya upasuaji, alisisitiza waziwazi kwamba hataki kutiwa damu mishipani, kupitia maneno na kupitia kadi ya Mwelekezo wa Kitiba. Lakini madaktari walipuuza maombi yake na kumtia damu mishipani mara kadhaa.

Mahakama ilikubali kwamba kukataa kutiwa damu mishipani “haihusu tu haki ya kujiamulia ni matibabu gani ambayo mtu angependa, bali pia ni jambo ambalo mtu anakataa kwa sababu ya dhamiri, iliyo na misingi imara ya imani ya kidini.” Mahakama hiyo ilifafanua haki hiyo kuwa “haki isiyopaswa kukiukwa, inayolindwa ‘kwa kiwango cha juu zaidi’ katika Katiba.”

Tangu 2015, hii ndiyo kesi ya kumi mfululizo ambayo Mashahidi wa Yehova wameshinda katika Mahakama Kuu ya Italia. Katika kila kesi, Mahakama iliunga mkono mambo muhimu yanayohusiana na uhuru wetu wa ibada. Kesi hizo zimehusu mambo yafuatayo:

  • Kukataa kutiwa damu mishipani: Mashahidi wa Yehova wangependa kupokea matibabu bora zaidi, na wanakubali aina nyingi sana za matibabu. Mahakama zimeamua kwamba wagonjwa ambao ni Mashahidi wanaweza kuchagua matibabu yanayopatana na dhamiri yao iliyozoezwa na kanuni za Biblia. Madaktari wanapaswa kuheshimu uamuzi wa mgonjwa kukataa kutiwa damu mishipani. Mgonjwa ana haki ya kisheria kufanya uamuzi huo kwa kutegemea imani yake ya kidini.

  • Malezi ya Mtoto: Wazazi ambao ni Mashahidi wana haki sawa na wazazi ambao si Mashahidi ya kuwafundisha watoto wao kuhusu mafundisho yao ya kidini.

  • Kutenga na ushirika: Mashahidi wa Yehova hawawabagui watu waliotengwa na ushirika. Badala yake, Mashahidi wako huru kukataa kushirikiana na watu walioondolewa katika makutaniko yao. Kufanya hivyo ni sehemu ya haki yao ya kidini ambayo inapaswa kuheshimiwa.

  • Kodi: Mashahidi wa Yehova hulipa kodi na majengo yao ya ibada yanapaswa kupewa haki na msamaha uleule wa kodi kama dini nyingine nchini Italia inapohusu maeneo ya kufanyia ibada.

Tunatiwa moyo wakati ambapo wenye mamlaka wanafanya maamuzi yanayolinda haki za watu wa Yehova zinazowawezesha kuabudu kwa uhuru.—Methali 21:1.