Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Timgad—Jiji Lililoangamia Lafichua Siri Zake

Timgad—Jiji Lililoangamia Lafichua Siri Zake

MVUMBUZI jasiri hakuamini macho yake. Alikuwa katika jangwa la Algeria ambapo kulikuwa na lango la ushindi la Waroma na sehemu fulani ya lango hilo ilikuwa imefukiwa mchangani! Mvumbuzi huyo alikuwa James Bruce kutoka Scotland na aligundua jambo hilo katika mwaka wa 1765. Hakujua kwamba alikuwa amesimama juu ya magofu ya jiji kubwa zaidi kuwahi kujengwa na Waroma, katika eneo lote la Kaskazini mwa Afrika. Jiji hilo la kale liliitwa Thamugadi, na sasa linajulikana kuwa Timgad.

Zaidi ya karne moja baadaye, katika mwaka wa 1881, wachimbuaji wa vitu vya kale kutoka Ufaransa walianza kufukua sehemu zilizobaki za jiji hilo. Wachimbuaji hao waligundua kwamba wakaaji wa jiji hilo la kale walifurahia maisha ya anasa na starehe licha ya kwamba waliishi kwenye mazingira magumu. Lakini ni nini kilichowachochea Waroma wajenge jiji hilo la kifahari katika eneo hilo? Na ni masomo gani tunayojifunza kutokana na jiji hilo la kale na wakaaji wake?

LENGO LA KIJANJA LA KISIASA

Waroma walipokuwa wakipanua milki yao katika eneo hilo la Kaskazini mwa Afrika, katika karne ya kwanza kabla ya kuja kwa Yesu Kristo, walipata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya makabila ya kuhamahama. Waroma wangefauluje kuishi kwa amani na wenyeji wa sehemu hiyo? Mwanzoni, Kikosi cha Tatu cha jeshi la Augusto kilijenga kambi nyingi zenye ngome na vituo vya walinzi katika eneo hilo kubwa lenye milima ambalo leo ni sehemu ya kaskazini ya nchi ya Algeria. Baadaye jeshi hilo lilijenga jiji la Timgad, lakini kwa sababu tofauti kabisa.

Waroma walijenga jiji la Timgad kwa ajili ya wanajeshi waliostaafu, lakini nia yao kuu ilikuwa kudhoofisha upinzani wa wenyeji. Mpango wao ulifaulu. Muda si muda maisha ya starehe katika jiji hilo yalianza kuwavutia wenyeji waliolitembelea ili kuuza bidhaa zao. Wakiwa na nia ya kukubaliwa kuishi jijini, ambako ni raia Waroma tu waliokubaliwa kuishi, wenyeji wengi walijiunga na Kikosi cha Jeshi la Roma kwa mkataba wa miaka 25 ili wao na watoto wao wapate uraia wa Roma.

Isitoshe, baadhi ya Waafrika hawakuridhika tu kupokea uraia wa milki ya Roma. Waafrika hao hata walipata vyeo vikubwa jijini Timgad na katika majiji mengine yaliyokuwa chini ya utawala wa Roma. Mbinu za kijanja za Waroma za kuwashawishi wenyeji wa sehemu hiyo washirikiane nao zilizaa matunda kwani miaka 50 tu baada ya kulijenga jiji la Timgad, Waafrika wengi kutoka Kaskazini mwa Afrika walikuwa wakiishi jijini humo.

JINSI WAROMA WALIVYOTEKA MIOYO YA WATU

Soko lenye barabara na maduka maridadi

Waroma walifauluje upesi kadiri hiyo kuteka mioyo ya wenyeji wa sehemu hiyo? Kwanza kabisa, waliendeleza  sera ya usawa miongoni mwa raia zao—sera ambayo ilianzishwa na mwanafalsafa Mroma aliyeitwa Cicero. Wanajeshi wa Roma waliostaafu na raia waliokuwa na asili ya Afrika walimiliki kiasi kilekile cha ardhi. Pia, jiji la Timgad lilijengwa kwa ustadi mkubwa sana. Nyumba zake zilikuwa na ukubwa wa mita 20 za mraba na zilitenganishwa na barabara nyembamba. Bila shaka mambo hayo yote yaliwavutia sana wakaaji wa jiji hilo.

Kama ilivyokuwa desturi katika majiji mengi ya Roma, wakaaji wa jiji walikutana katika siku za soko zilizokuwa na shughuli nyingi ili wapate habari mpya mpya au ili kucheza tu michezo fulani. Hapana shaka kwamba wenyeji waliokuwa wakiishi kwenye milima iliyokuwa karibu na jiji hilo walikuwa wakijiwazia wakitembea kwenye barabara za jiji hilo zenye vivuli katika siku zenye joto na jua kali, au walijiwazia wakiburudika kwenye mojawapo ya mabafu mengi ya umma yasiyotozwa malipo huku wakifurahia sauti ya maji yaliyokuwa yakitiririka. Labda hata walijiwazia wakiwa wameketi kuzunguka mabubujiko ya maji huku wakipiga gumzo na marafiki zao. Kwa kweli, walitamani sana maisha hayo yenye kuvutia.

Jiwe la kaburi lenye michongo ya miungu

Jumba la maonyesho pia lilichangia kwa kiasi kikubwa kuteka mioyo ya watu. Jumba hilo lilikuwa na uwezo wa kutoshea zaidi ya watu 3,500. Wahudhuriaji wenye kelele kutoka jiji la Timgad na miji iliyokuwa karibu walijazana kwenye jumba hilo ili kujionea maonyesho mbalimbali. Jukwaani, waigizaji waliwatumbuiza wahudhuriaji kwa michezo ya Kiroma ambayo mara nyingi ilikuwa na jeuri na upotovu wa maadili.

Pia, dini ya Waroma haikuachwa nyuma. Sakafu na kuta za mabafu zilipambwa kotekote kwa michoro iliyoonyesha hekaya za wapagani. Kwa kuwa kuoga kulikuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, wakaaji walianza hatua kwa hatua kuzoea dini na miungu ya Waroma kupitia michoro hiyo. Mbinu ya kuwafanya Waafrika waige utamaduni na desturi za Waroma ilifaulu kwani muda si muda ilikuwa kawaida kurembesha mawe ya makaburi kwa michongo iliyokuwa na miungu ya wenyeji na ile ya Waroma.

JIJI MARIDADI LASAHAULIKA

Baada ya Maliki Trajani kuanzisha jiji hilo katika mwaka wa 100 W.K., Waroma walianzisha miradi ya kuzalisha mafuta ya zeituni, divai, na nafaka katika eneo lote la Kaskazini mwa Afrika. Punde si punde eneo hilo likawa kama ghala kwa ajili ya milki nzima ya Roma, likitosheleza mahitaji ya milki hiyo kwa kutokeza bidhaa hizo muhimu. Kama ilivyokuwa na majiji mengine yaliyotawaliwa na Waroma, Timgad pia lilistawi. Baada ya muda, idadi ya watu katika jiji hilo iliongezeka, hali iliyosababisha jiji hilo lipanuke.

Wakaaji wa jiji hilo na wale waliomiliki ardhi walipata ufanisi mkubwa kwa sababu ya kufanya biashara na Waroma, hata hivyo wakulima wenyeji walikandamizwa kwa kupokea faida kidogo. Katika karne ya 3 W.K., ukosefu wa haki na kodi za juu ziliwafanya wakulima wenye mashamba madogo waanze kuleta vurugu. Baadhi ya wakulima hao waliokuwa Wakatoliki, waliamua kuwa Wadonati. Wadonati walikuwa Wakristo ambao waliamua kuachana na Ukatoliki kwa sababu ya uongozi mbaya katika kanisa hilo.—Ona sanduku lenye kichwa “ Wadonati—‘Kanisa Lenye Dosari.’

 Baada ya karne kadhaa za mizozo ya kidini, vita vya wenyewe kwa wenyewe, na uvamizi kutoka kwa maadui wakatili, ustaarabu wa Waroma uliporomoka katika eneo hilo la Kaskazini mwa Afrika. Kufikia karne ya 6 W.K., Waarabu wenyeji waliliteketeza kabisa jiji la Timgad nalo likasahaulika kwa zaidi ya miaka 1,000.

“HAYA NDIYO MAISHA!”

Maneno ya Kilatini yaliyofukuliwa yanayosema: “Kuwinda, kuoga, kucheza, kucheka—haya ndiyo maisha!”

Wachimbuaji wa vitu vya kale waliofukua magofu ya jiji la Timgad walichekeshwa na maandishi ya Kilatini waliyoyapata sehemu hiyo. Maandishi hayo yanasema: “Kuwinda, kuoga, kucheza, kucheka—haya ndiyo maisha!” Mwanahistoria mmoja kutoka Ufaransa alisema kwamba maneno hayo “yanaunga mkono falsafa ambayo haina lengo hususa, ingawa baadhi ya watu watasema huo ndio mwendo wenye hekima maishani.”

Ukweli wa mambo ni kwamba wakati fulani Waroma waliishi maisha ya namna hiyo. Paulo, mtume Mkristo aliyeishi katika karne ya kwanza alizungumzia kuhusu watu ambao walisema: “Na tule na tunywe, kwa maana kesho tutakufa.” Hilo ndilo lililokuwa lengo kuu maishani mwao. Ingawa walikuwa wafuasi wa dini, Waroma walipenda anasa na hawakuzingatia maana au kusudi la maisha. Paulo aliwaonya Wakristo wenzake wajilinde dhidi ya watu wa namna hiyo aliposema: “Msipotoshwe. Mashirika mabaya huharibu tabia nzuri.”—1 Wakorintho 15:32, 33.

Ingawa watu walioishi katika jiji la Timgad waliishi karibu miaka 1,500 hivi iliyopita, maoni ya watu kuhusu maisha hayajabadilika sana tangu wakati huo. Watu wengi leo huishi kwa kutegemea tu mambo wanayoona sasa. Watu hao wanaunga mkono maisha ambayo Waroma walikuwa nayo bila kujali hatari za kufuata mtindo huo wa maisha. Hata hivyo, Biblia inatueleza mambo waziwazi inaposema: “Tamasha ya ulimwengu huu inabadilika.” Kwa hiyo inatuhimiza ‘tusiutumie ulimwengu kwa ukamili.’—1 Wakorintho 7:31.

Magofu ya jiji la kale la Timgad ni ushahidi tosha kwamba kuwa na furaha na kusudi maishani hakutegemei tu kuwinda, kuoga, kucheza, na kucheka. Badala yake, kunategemea kufuata ushauri huu wa Biblia unaosema: “Ulimwengu unapitilia mbali na pia tamaa yake, lakini yeye anayefanya mapenzi ya Mungu anadumu milele.”—1 Yohana 2:17.