Mwanzo 39:1-23

  • Yosefu katika nyumba ya Potifa (1-6)

  • Yosefu ampinga mke wa Potifa aliyekuwa akimshawishi (7-20)

  • Yosefu akiwa gerezani (21-23)

39  Basi Yosefu akapelekwa Misri,+ na Mmisri aliyeitwa Potifa,+ ofisa wa makao ya Farao aliyekuwa pia mkuu wa walinzi, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli+ waliomleta huko.  Lakini Yehova alikuwa pamoja na Yosefu.+ Kwa hiyo akafanikiwa na kuwekwa kuwa msimamizi wa nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.  Bwana wake akaona kwamba Yehova alikuwa pamoja naye na kwamba Yehova alikuwa akifanikisha kila jambo alilokuwa akifanya.  Yosefu akaendelea kupata kibali machoni pa Potifa, naye akawa mhudumu wake binafsi. Kwa hiyo Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, na wa vitu vyake vyote.  Tangu alipomweka kuwa msimamizi wa nyumba yake na wa vitu vyake vyote, Yehova aliendelea kuibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu, na Yehova akabariki vitu vyote alivyokuwa navyo nyumbani na shambani.+  Hatimaye akamwachia Yosefu usimamizi wa vitu vyake vyote, naye hakujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula chake. Isitoshe, Yosefu akawa mwanamume mwenye umbo zuri na sura inayopendeza.  Sasa baada ya hayo, mke wa bwana wake akaanza kumtupia jicho Yosefu na kumwambia: “Lala nami.”  Lakini akakataa na kumwambia mke wa bwana wake: “Tazama, bwana wangu hajui vitu nilivyo navyo nyumbani, naye ameniweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote.  Hakuna yeyote aliye mkuu zaidi yangu katika nyumba hii, naye hajanikataza kitu chochote isipokuwa wewe, kwa sababu wewe ni mke wake. Basi ninawezaje kufanya uovu huu mkubwa na kwa kweli nimtendee Mungu dhambi?”+ 10  Basi siku baada ya siku alizungumza na Yosefu, lakini Yosefu hakukubali kamwe kulala naye wala kukaakaa naye. 11  Lakini siku moja kati ya siku ambazo Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake, hakukuwa na mtumishi yeyote nyumbani. 12  Basi mke wa Potifa akaishika kwa nguvu nguo ya Yosefu akisema: “Lala nami!” Lakini Yosefu akaiacha nguo yake mikononi mwake na kukimbilia nje. 13  Mara tu mke wa Potifa alipoona kwamba Yosefu ameiacha nguo yake mikononi mwake na kukimbilia nje, 14  akaanza kulia kwa sauti kubwa na kuwaita wanaume wa nyumbani mwake na kuwaambia: “Tazameni! Alituletea mwanamume huyu Mwebrania ili tuwe kichekesho. Alikuja kulala nami, lakini nikaanza kulia kwa sauti yangu yote. 15  Mara tu aliposikia nikilia kwa sauti kubwa na kupiga mayowe, akaiacha nguo yake kando yangu na kukimbilia nje.” 16  Kisha mke wa Potifa akaiweka nguo ya Yosefu kando yake mpaka bwana wake* aliporudi. 17  Halafu akamsimulia kisa hicho, akisema: “Yule mtumishi Mwebrania uliyetuletea alikuja kunifanya mimi niwe kichekesho. 18  Lakini mara tu nilipoanza kulia kwa sauti kubwa na kupiga mayowe, aliacha nguo yake kando yangu na kukimbilia nje.” 19  Punde tu bwana wa Yosefu alipomsikia mke wake akisema: “Hayo ndiyo mambo ambayo mtumishi wako alinitendea,” akawaka hasira. 20  Basi bwana wa Yosefu akamchukua Yosefu na kumtupa gerezani, mahali ambapo wafungwa wa mfalme walifungwa, akabaki humo gerezani.+ 21  Lakini Yehova aliendelea kuwa pamoja na Yosefu, naye akazidi kumtendea kwa upendo mshikamanifu na kumfanya apate kibali machoni pa ofisa mkuu wa gereza.+ 22  Kwa hiyo, ofisa mkuu wa gereza akamweka Yosefu kuwa msimamizi wa wafungwa wote gerezani, na wa kazi zote walizokuwa wakifanya humo, yeye ndiye aliyehakikisha zimefanywa.+ 23  Ofisa mkuu wa gereza hakujishughulisha na jambo hata moja lililokuwa chini ya usimamizi wa Yosefu, kwa maana Yehova alikuwa pamoja na Yosefu na Yehova alifanikisha jambo lolote alilofanya.+

Maelezo ya Chini

Yaani, bwana wa Yosefu.